TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU MALALAMIKO
YALIYOFIKISHWA KWENYE KAMATI DHIDI YA WAHESHIMIWA WABUNGE SUZAN LYIMO (MB) NA
ANATROPIA THEONEST (MB)
KUTOKANA NA KUTUHUMIWA KUSEMA UONGO NA
KUTOA TAARIFA AMBAZO HAZINA
UKWELI BUNGENI
_________________
1.0
UTANGULIZI
1.1
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 4 fasili (2) na (3) ya
Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 naomba
kuwasilisha Mbele ya Bunge lako Tukufu Taarifa ya Kamati kuhusu shauri la Mhe.
Susan A. Lyimo (Mb) na Mhe. Anatropia Theonest (Mb) kudaiwa kusema uongo
Bungeni.
1.2
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kukushukuru wewe binafsi
kwa ujasiri mkubwa ulionao katika kuliongoza
Bunge letu kwa ufanisi mkubwa.
1.3
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 17 Mei, 2016, kwa mujibu wa Kanuni
ya 4(1) (a) na (b) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la
Januari, 2016 ulipeleka malalamiko
ya baadhi Wabunge mbele ya Kamati ili
iyachunguze na kutoa mapendekezo yake kuhusiana na malalamiko hayo. Wabunge
waliolalamika walieleza kuwa walalamikiwa walisema uongo Bungeni na kutoa
taarifa ambazo hazina ukweli kinyume na Kanuni ya 63(1) na 64(1)(a) ya Kanuni
za Kudumu za Bunge.
1.4
Mheshimiwa
Spika, Wabunge
waliowasilisha malalamiko ni Mheshimiwa Yusuph Hamad Masauni (Mb) Naibu Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, aliyemlalamikia Mhe. Suzan Lyimo (Mb) na Mheshimiwa William Lukuvi (Mb), Waziri wa
Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi
aliyemlalamikia Mheshimiwa Anatropia Theonest (Mb).
1.5
Mheshimiwa
Spika, baada
ya maelekezo hayo taratibu za kuanza
kusikiliza shauri hili zilifanyika ikiwa ni pamoja na kuwaita mashahidi kwa Hati
za Wito. Hati hizo zilielekeza kuwa waheshimiwa hao walitakiwa kufika mbele ya Kamati ili kutoa ufafanuzi
kuhusu malalamiko yao na Wabunge waliolalamikiwa walitakiwa kufika mbele ya
Kamati ili waweze kueleza ni kwa nini
wasichukuliwe hatua kwa kukiuka Kanuni ya 63 (1) na 64 (1) (a) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.
1.6
Mheshimiwa Spika, taarifa ambazo zinazodaiwa kuwa ni za uongo zilitolewa kwa nyakati tofauti
katika Bunge la Kumi na Moja ambapo, katika tukio la kwanza Mheshimiwa Anatropia
Theonest (Mb) alituhumiwa kutoa kauli katika Mkutano wa Pili wa Bunge la Kumi na
Moja na matukio mengine ni katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja
unaoendelea hivi sasa.
2.0 CHIMBUKO LA SHAURI LA MALALAMIKO YA MHE.
YUSUPH HAMAD MASAUNI (MB), NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI DHIDI YA MHE.
SUZAN LYIMO (MB)
2.1
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 12 Mei, 2016, Mhe. Yusuph Hamad Masauni
(Mb), aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni ya 68(7) na 64(1) (a) kuwa siku
ya tarehe 11 Mei, 2016 wakati wa mjadala wa Hotuba ya Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Watoto na Wazee Mhe. Suzan Lyimo (Mb) alisema uongo Bungeni.
2.2
Mheshimiwa Spika, akijenga hoja yake Mhe. Masauni (Mb) alisema
kuwa Mhe. Suzan Lyimo (Mb) alipokuwa akichangia alitoa kauli kwamba, kuna
magari 777 ya washawasha ya polisi yameingizwa nchini, taarifa za uhakika
alizonazo kama Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ni kwamba, magari ya washawasha yaliyonunuliwa ni 32 tu
na sio 777 yaliyotajwa na Mhe. Susan Lyimo.
2.3
Mheshimiwa Spika, Mhe. Masauni (Mb) aliomba mwongozo wa Kiti kwamba ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa na Bunge
kutokana na maelezo hayo ya uongo Bungeni.
2.4
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kumbukumbu Rasmi za Bunge za tarehe
11 Mei, 2016 Mhe. Suzan Lyimo(Mb) alinukuliwa akisema kama ifuatavyo;
“Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kama
wakinamama kukubali hali hii
iendelee na nasema hivi kwa sababu nchi hii ina uwezo kama tuliweza kununua
magari ya washawasha narudia, kama tuliweza kununua magari ya washawasha 777
ambayo ni 50 tu yalitumika kwenye uchaguzi na gari moja nime-google kwa Alibaba
ambao ndio wanaleta magari, gari moja lina gharama ya shilingi milioni 150
mpaka 400 lakini tuchukue wastani wa dola laki tatu kwa moja. Inamaana kwa
magari 700 ni dola laki mbili na kumi milioni ukizipeleka kwenye hela za
kitanzania ni bilioni 420, bilioni 420 kwa kata 3990 tulizonazo Tanzania nzima
na ambulance, ambayo ambulance moja nime-google vilevile ambayo tena ni advance
inaenda kwa shilingi milioni 105 ukigawanya ina maana kila kata hapa Tanzania
ingepata ambulance (Makofi).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo,
tunajiuliza priorities za nchi hii ni
zipi, ni afya ya mtanzania au kitu gani? Kwa sababu kama ni suala nimesema
magari 77 ya washawasha yangeweza kubaki, tunazungumzia yale 700 yaliyobaki
yaani yangetosha ambulance. (Makofi).
2.5 Mheshimiwa
Spika, kufuatia ombi hilo la mwongozo
lililoombwa na Mhe. Masauni, Mhe. Spika alielekeza kuwa, kwa kuwa Mhe. Suzan
Lyimo (Mb) hakuwepo ukumbini wakati mwongozo ulipoombwa, hivyo atakaporudi
katika kikao cha jioni atatakiwa kufuta kauli yake au kutoa uthibitisho ndani ya
Bunge.
2.5
Mheshimiwa Spika, katika kikao cha jioni cha siku tajwa, Mheshimiwa
Spika alimtaka Mhe. Suzan Lyimo kufuta maneno aliyoyatoa au kuthibitisha kauli
yake na Mhe. Lyimo alionekana kuwa tayari kuthibitisha. Kwa kuwa uthibithisho
wake ulielekea kuwa ungeweza kuchukua muda mrefu, Mheshimiwa Spika alimtaka
Mhe. Lyimo awasilishe uthibitisho wake kwa maandishi na kwamba Spika
angewasilisha uthibitisho huo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge. Mhe. Lyimo aliwasilisha uthibitisho wake wa maandishi kama alivyotakiwa
na Spika.
3.0 HADIDU ZA REJEA NA HOJA ZA
MSINGI (ISSUES)
3.1 Mheshimiwa Spika, Katika Waraka wa Spika
wa kuleta shauri kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ulirejea
Kanuni ya 4(1) (a) na (b) ya Nyongea ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo
la Januari 2016. Kwa urahisi wa rejea nanukuu Kanuni hiyo:
4(1)
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
itatekeleza majukumu yafatayo:-
(a)
Kuchunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala
yote ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge yatakayopelekwa na Spika;
(b)
Kushughulikia mambo yanayohusu maadili ya wabunge
yatakayopelekwa na Spika
4.0
UCHAMBUZI WA KAMATI KUHUSU MALALAMIKO
YA MHESHIMIWA YUSSUF HAMAD MASAUNI (MB)
DHIDI YA MHESHIMIWA SUZAN LYIMO (MB)
4.1
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu waraka uliouwasilisha mbele ya Kamati
na kwa kuzingatia maudhui yaliyo katika malalamiko ya Wabunge waliowasilisha malalalamiko yao Kamati
inajukumu la kuchunguza kwa kujiuliza hoja mbili ambazo ni:-
(a)
Iwapo Mheshimiwa Suzan Lyimo (Mb) alisema uongo au kutoa taarifa ambazo
hazina ukweli kinyume na Kanuni ya 63 (1) na 64(1) (a) ya Kanuni za Kudumu za
Bunge, Toleo la Januari, 2016.
(b)
Ikiwa hoja (a) itathibitika, ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa kwa
mujibu wa Kanuni za Bunge.
4.2
Mheshimiwa Spika, katika kufanya uchambuzi wake kuhusu suala hili, Kamati imefanya rejea
zifuatazo;
(i)
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
(ii)
Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
(iii)
Kumbukumbu Rasmi za Bunge za Tarehe 3 Februari, 2016, tarehe 10 na 11
Mei, 2016.
(iv)
Uthibitisho uliowasilishwa na Mbunge aliyetakiwa kuwasilisha
uthibitisho huo.
(v)
Mahojiano na Mashahidi waliofika mbele ya Kamati.
4.3
Mheshimiwa Spika Kanuni za Bunge zilizotungwa chini ya Ibara ya
89(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeweka utaratibu maalum
unaopaswa kutumika kwa mambo yote yanayohusu uendeshaji wa Bunge. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuweka Kanuni za
majadiliano Bungeni.
4.4
Mheshimiwa Spika, Kanuni za Kudumu za Bunge zimeweka masharti kuhusu
maneno au taarifa zinazoruhusiwa kutolewa Bungeni. Kanuni ya 63 (1) na 64(1)(a) za Kanuni za
Kudumu za Bunge zimekataza Mbunge yeyote kutoa taarifa au kusema uongo Bungeni
na zinamtaka Mbunge kusema au kutoa taarifa ambazo ana uhakika nazo. Kwa urahisi wa rejea nanukuu Kanuni hizo kama
ifuatayo;-
“63(1) Bila kuathiri masharti ya
Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano
katika Bunge, ni marufuku kabisa kusema uongo Bungeni na kwa sababu hiyo, Mbunge
yeyote anapokuwa akisema Bungeni ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli
au maelezo kuhusu jambo au suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni la kweli
na siyo jambo la kubuni au la kubahatisha tu”
“64(1) (a) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya
100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika
Bunge, Mbunge:-
(a)
Hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina
ukweli”
5.0 MAHOJIANO
KATIKA SHAURI LA MHE. HAMAD MASAUNI (MB) DHIDI YA MHE. SUZAN LYIMO (MB)
5.1 Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 31
Mei, 2016, Kamati ilipata fursa ya kumhoji Mhe. Hamadi Masauni (Mb) kuhusiana
na malalamiko yake dhidi ya Mhe. Suzan Lyimo (Mb). Mhe. Masauni alieleza kuwa alipokuwa
akichangia mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Watoto na Wazee Mhe. Suzan Lyimo (Mb) alieleza kuwa Serikali imenunua Magari ya
Washawasha 777 badala ya kununua MRI na CT Scaners. Mhe. Masauni alieleza kuwa mchango
huo ulilenga kupotosha jamii kwani Serikali haijanunua idadi hiyo ya magari ya
washawasha bali Magari 777 ni mpango wa Serikali wa kuboresha Jeshi la Polisi
kwa kulipatia vitendea kazi ikiwemo magari. Magari 777 yanayotarajiwa
kununuliwa ambapo baadhi yamekwishapokelewa ni kwa ajili ya matumizi mbalimbali
ya Jeshi la Polisi na kwamba kati ya
Magari hayo, 32 tu ndiyo magari ya washawasha na mengine ni kwa ajili ya
matumizi mbalimbali ya kipolisi ikiwemo ya oparesheni za polisi, doria, zimamoto na kadhalika.
5.2 Mheshimiwa
Spika, Mhe. Hamad Masauni (Mb) alipohojiwa kuhusu majibu
yake katika Swali la Nyongeza lililoulizwa na Mhe. Suzan Lyimo kuhusu idadi
hiyo ya magari ya washawasha alieleza kuwa, katika kujibu swali la nyongeza hakusema kuwa
Serikali imenunua magari ya Washawasha 777. Mhe. Masauni alirejea Hansard ya
tarehe 4 Februari, 2016 ambayo inasomeka
Nanukuu
“Si kweli kwamba magari ya washawasha yamenunuliwa na
hayana tija. Magari ya washawasha yamenunuliwa ikiwa ni miongoni mwa ile
program ya kununua magari 777, kwa ajili ya matumizi ya askari kwa hiyo magari
haya yanasaidia sana na bado mengine yatafika kwa ajili ya shughuli mbalimbali
za polisi”
5.3 Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Masauni
aliieleza Kamati kuwa majibu aliyoyatoa hayaelezi kuwa Serikali imenunua Magari
777 ya Washawasha bali inaeleza kuwa magari hayo siyo washawasha pekee bali ni
kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya Jeshi la Polisi. Kutokana na maelezo hayo, Mheshimiwa Masauni
aliieleza Kamati kuwa Mhe. Suzan Lyimo alisema uongo Bungeni.
5.4 Mheshimiwa Spika, Kamati ilipata fursa
ya kumhoji Mhe. Suzan Lyimo kuhusiana na malalamiko ya Mhe. Yusuph Masauni.
Mhe. Suzan Lyimo aliieleza Kamati kuwa aliwasilisha utetezi wake kwa Spika.
Kamati iliupata utetezi wake. Utetezi huo umegawanyika katika sehemu tatu
ambazo ni:
(i)
Ripoti kutoka vyombo vya habari kama Jamii Forum na Gazeti la Mwananchi
Online
(ii)
Hansard ya Bunge kuhusu majibu ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi Mhe. Eng. Masauni ya tarehe 04/02/2016 alipokuwa akijibu swali ya nyongeza
kuhusu ununuzi wa Magari ya washawasha 777 badala ya kununua CT-Scaners na MRI
pesa ambayo ingetosha kununua mashine hizo kwa hospitali zote za rufaa nchi
nzima.
(iii)
Mtandao wa Alibaba ambao ni Wakala wa Kimataifa wa kuuza bidhaa
mbalimbali yakiwemo magari ya aina zote.
5.5 Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Suzan Lyimo
(Mb) alipofika mbele ya Kamati alieleza kuwa katika vielelezo alivyowasilisha. Pia
kuna taarifa kutoka
Habarikablog.blogspot.com. Kamati ilipofanya uchambuzi wa vielelezo hivyo,
ilibaini kwamba katika vielelezo hivyo hakukuwa na Kielelezo cha Mwananchi
online bali Mwanahalisi Online. Aidha, katika vielelezo alivyowasilisha kwa
Spika kielelezo cha Habarikablog.blogspot.com hakikuainishwa.
5.6 Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Suzan Lyimo
(Mb) aliieleza Kamati kuwa alirejea Kanuni ya 63(2) ya Kanuni za Kudumu za
Bunge, Toleo la 2016 kwamba Mbunge hatachukuliwa kuwa anasema uongo iwapo
anafanya rejea ya habari kuhusu jambo fulani lililotangazwa au lililoandikwa na
vyombo vya habari. Hivyo alisisitiza kuwa kauli alizozisema Bungeni hazikuwa za
uongo kwa kuwa alifanya rejea ya vyombo vya Habari alivyovitaja.
5.8 Mheshimiwa Spika, Kamati ilijiuliza swali
moja la msingi kuhusiana na shauri hili, nalo ni Je? Mhe. Suzan Lyimo alisema
uongo Bungeni kinyume na Kanuni ya 64(1) kama alivyolalamikiwa na Mhe. Yussuf
H. Masauni (Mb).
5.9 Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Kanuni ya 64(1) ya Kanuni za Kudumu
za Bunge kama ilivyonukuliwa katika taarifa hiyo, Mbunge yoyote haruhusiwi
kusema uongo Bungeni.
5.10 Mheshimiwa
Spika, Kanuni za Kudumu za Bunge hazijaeleza zipi ni habari zenye sifa ya
kuwa na ukweli. Hata hivyo, Kanuni ya 63(1) inaeleza kuwa Mbunge anatakiwa
kutoa Bungeni taarifa ambazo ana uhakika nazo na si za kubahatisha tu. Kwa
maana nyingine Mbunge anapaswa kutoa taarifa ambazo amezifanyia utafiti na kuwa
na uhakika na jambo ambalo analizungumza.
5.11 Mheshimiwa
Spika, majibu ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Yussuf Hamad
Masauni (Mb) hayaelezi kuwa Serikali imenunua Magari 777 ya Washawasha bali
inasema magari hayo yamenunuliwa kwa ajili ya matumizi ya askari na kwa ajili
ya shughuli mbalimbali za kipolisi. Aidha Naibu Waziri ameeleza kuwa kati ya
Magari hayo, ni 32 tu ndiyo ya washawasha.
Mheshimiwa Spika, Aidha, katika vielelezo vyote vilivyowasilishwa
na Mhe. Suzan Lyimo, hakuna kielelezo hata kimoja kinachothibitisha kuwa
Serikali imenunua magari ya washawasha 777 jambo ambalo lina dhihirisha kuwa
alisema uongo Bungeni.
5.12 Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo
hayo na kwa mujibu wa masharti ya Kanuni za Bunge Kamati inamtia hatiani Mheshimiwa Suzan Lyimo kwa Kusema uongo
Bungeni.
5.13 Mheshimiwa Spika, baada ya Kumtia
hatiani Mheshimiwa Suzan Lyimo (Mb) na kwa kuzingatia Kanuni ya 63(8) ya Kanuni
za Kudumu za Bunge, Kamati inapendekeza mbunge huyu kupewa adhabu ifuatayo:-
Katika kupendekeza adhabu Kamati ilizingatia kuwa Mhe. Suzan Lyimo ni
kosa lake la kwanza na alitoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati pamoja na
kutekeleza kikamilifu maelekezo ya Kiti cha Spika.
Hata hivyo, Kamati ilizingatia pia kuwa Mhe. Suzan Lyimo ni mzoefu
katika shughuli za Bunge na anaelewa vyema masharti ya Kanuni za Bunge, kwa
msingi huo Kamati inaliomba Bunge lako tukufu likubali pendekezo la Kamati la
kumsimamisha Mhe. Suzan Lyimo (Mb) asihudhurie vikao vitano (5) vya Bunge
mfululizo kuanzia tarehe 17 Juni, 2016 hadi tarehe 24 Juni, 2016.
2.2.1 CHIMBUKO
LA MALALAMIKO YA MHE. WILLIAM V. LUKUVI
(MB) DHIDI YA MHE. ANATROPIA THEONEST (MB)
2.2.2 Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 4
Februari, 2016 Mhe. William Lukuvi (Mb)
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwasilisha katika Meza ya
Spika katika Ukumbi wa Bunge barua ya malalamiko akilalamikia kuwa mnamo
3 Februari, 2016 katika Mkutano wa Pili,
Kikao cha Saba, Bunge la Kumi na Moja wakati wa majadiliano kuhusu
Kamati ya Mipango, Mhe. Anatropia Theonest wakati alipokuwa akichangia kuhusu
Kamati ya Mipango alisema uongo Bungeni kwa kudai kuwa yeye Mhe. Lukuvi, akiwa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mwaka 2011 alihusika na uporaji wa viwanja
walivyopewa waathirika wa mabondeni na kwamba jambo hilo kweli kwa kuwa Mwaka
2011, Mhe. Lukuvi hakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam bali alikuwa Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.
2.2.3 Mheshimiwa Spika, Mhe. Lukuvi katika maombi
ya mwongozo alikitaka kiti kimtake Mhe. Anatropia Theonest kufuta kauli yake au
arekebishe kauli yake. Kwa namna moja au nyingine barua hiyo haikumfikia Spika
hivyo, Mhe. Lukuvi aliandika tena barua nyingine mwezi Mei, 2016 kukumbushia
kuhusu malalamiko yake ili yafanyiwe kazi.
2.2.4 Mheshimiwa
Spika, Malalamiko ya Mhe. Lukuvi yanatokana na mchango wa Mhe. Anatropia Theonest alipokuwa akichangia
Bungeni mnamo tarehe 3 Februari, 2016 wakati wa majadiliano kuhusu Kamati ya
Mipango ambapo alieleza yafuatayo:
…”.Natokea katika jiji la Dr es salaam ambalo
limekuwa na migogoro mikubwa ya ardhi.
Wananchi zaidi ya kaya 16000 zimewekewa alama “x” kwamba, kwenye mabonde,
wanaenda kubomolewa majumba yao. Zaidi
ya wananchi 99,000 watakuwa ni watu wasio na makazi. Changamoto ni kwamba
serikali ilikuwepo, watendaji walikuwepo, Waziri Lukuvi ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa
wa Dar es salaam alifanya nini wakati wote ambapo wananchi wameishi katika
maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 1998
yalitengwa maeneo ya Tegeta ili wananchi waliokuwa wanaishi mabondeni wahamie, hali
kadhalika mwaka 2011 akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam. Wananchi wa Jimbo la
Segerea, wananchi wa Ilala, wanataka viwanja vyao kwa sababu wanasema anahusika
katika uporaji wa maeneo waliyopewa wananchi waliokuwa wanaishi mabondeni.”
2.2.5 Mheshimiwa Spika, katika malalamiko yake Mhe.
William Lukuvi (Mb) Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alieleza
kuwa tuhuma zilizotolewa na Mhe. Anatropia kumhusisha na uporaji wa maeneo
waliyopewa wananchi wa Jimbo la Ilala na Segerea walokuwa
wanaishi mabondeni siyo za kweli
kwani mwaka 2011 alikuwa ni Waziri wa Nchi na hakuhusika katika tuhuma
hizo na wakati huo hakuwa Mkuu wa Mkoa.
6.0
HADIDU ZA REJEA NA HOJA ZA MSINGI (ISSUES)
6.1
Mheshimiwa Spika, Katika Waraka wa Spika wa kuleta shauri kwa Kamati
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ulirejea Kanuni ya 4(1) (a) na (b) ya
Nyongea ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016. Kwa
urahisi wa rejea nanukuu Kanuni hiyo:
4(1)
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
itatekeleza majukumu yafatayo:-
(c)
Kuchunguza na kutoa mapendekezo khusu masuala yote
ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge yatakayopelekwa na Spika;
(d)
Kushughulikia mambo yanayohusu maadili ya wabunge
yatakayopelekwa na Spika
7.0
UCHAMBUZI WA KAMATI KUHUSU MALALAMIKO
YA MHESHIMIWA WILLIAM LUKUVI (MB) DHIDI YA MHESHIMIWA ANATROPIA THEONEST (MB)
7.1
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu waraka uliouwasilisha mbele ya Kamati
na kwa kuzingatia maudhui yaliyo katika malalamiko ya Wabunge waliowasilisha malalalamiko yao Kamati
inajukumu la kuchunguza kwa kujiuliza hoja mbili ambazo ni:-
(a)
Iwapo Mheshimiwa Anatropia Theonest (Mb) alisema uongo au kutoa taarifa
ambazo hazina ukweli kinyume na Kanuni ya 63 (1) na 64(1) (a) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.
(b)
Ikiwa hoja (a) itathibitika, ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa kwa
mujibu wa Kanuni za Bunge.
7.2
Mheshimiwa Spika, katika kufanya uchambuzi wake kuhusu suala hili, Kamati imefanya rejea
zifuatazo;
(vi)
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
(vii)
Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
(viii)
Kumbukumbu Rasmi za Bunge za Tarehe 3 Februari, 2016, tarehe 10 na 11
Mei, 2016.
(ix)
Uthibitisho uliowasilishwa na Mbunge aliyetakiwa kuwasilisha
uthibitisho huo.
(x)
Mahojiano na Mashahidi waliofika mbele ya Kamati.
7.3
Mheshimiwa Spika Kanuni za Bunge zilizotungwa chini ya Ibara ya
89(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeweka utaratibu maalum
unaopaswa kutumika kwa mambo yote yanayohusu uendeshaji wa Bunge. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuweka Kanuni za
majadiliano Bungeni.
7.4
Mheshimiwa Spika, Kanuni za Kudumu za Bunge zimeweka masharti kuhusu
maneno au taarifa zinazoruhusiwa kutolewa Bungeni. Kanuni ya 63 (1) na 64(1)(a) za Kanuni za
Kudumu za Bunge zimekataza Mbunge yeyote kutoa taarifa au kusema uongo Bungeni
na zinamtaka Mbunge kusema au kutoa taarifa ambazo ana uhakika nazo. Kwa urahisi wa rejea nanukuu Kanuni hizo kama
ifuatayo;-
“63(1) Bila kuathiri masharti ya
Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano
katika Bunge, ni marufuku kabisa kusema uongo Bungeni na kwa sababu hiyo, Mbunge
yeyote anapokuwa akisema Bungeni ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli
au maelezo kuhusu jambo au suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni la kweli
na siyo jambo la kubuni au la kubahatisha tu”
“64(1) (a) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya
100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika
Bunge, Mbunge:-
(b)
Hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina
ukweli”
8.0 MAHOJIANO
KATIKA SHAURI LA MHESHIMIWA WILLIAM LUKUVI DHIDI YA MHE. ANATROPIA THEONEST
8.1 Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa William
Lukuvi (Mb), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alifika mbele ya
Kamati Mnamo tarehe 1 Juni, 2016 kama Hati yake ya Wito ilivyomtaka. Baada ya kufika aliieleza Kamati kuwa Mhe.
Anatropia Theonest (Mb) alipokuwa akichangia katika Kamati ya Mipango,
alilieleza Bunge na Umma wa watanzania kuwa yeye Mhe. Lukuvi (Mb) alipokuwa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alihusika katika kupora viwanja vilivyokuwa
vimetengwa kwa ajili ya waathirika wa Mafuriko. Mhe Lukuvi aliieleza kamati
kuwa jambo hilo si la kweli kwani Mwaka 2011 yeye hakuwa Mkuu wa Mkoa bali
alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.
8.2 Mheshimiwa
Spika, Aidha, Mhe. Lukuvi
aliieleza Kamati kuwa taarifa zilizotolewa na Mhe. Anatropia si tu kwamba zilikuwa za uongo
bali zimemfedhehesha sana kwa kuhusishwa na uporaji wa viwanja vya watu
wanyonge na kwamba jambo hilo limemdhalilisha mbele ya jamii kwa kudhaniwa kuwa
anajihusisha na uporaji wa ardhi.
8.3 Mheshimiwa
Spika, wakati wa mahojiano na Kamati Mhe. Anatropia Theonest alikiri
mbele ya Kamati kuwa alisema uongo Bungeni kwa kuwa, ni kweli Mhe.
Luvuvi hakuwa Mkuu wa Mkoa Mwaka
2011 hivyo asingeweza kuhusika na uporaji wa viwanja vya waathirika wa
mafuriko. Aidha, alieleza iwapo kama angeambiwa jambo hilo akiwa
Bungeni, kuwa kauli aliyokuwa ameitoa siku hiyo ilikuwa
ya uongo angeweza kuifuta. Alionesha kusikitika kuona kuwa suala
hili limefika Kamati ya Maadili ambalo lingeweza kumalizika ndani ya
Ukumbi wa
Bunge ikiwa angepata fursa.
8.4 Mheshimiwa
Spika, katika maelezo ya kuthibitisha kuhusu tuhuma hizo kama alivyotakiwa
kufanya alieleza kuwa utaratibu uliowekwa na Kanuni ya 63 haukufutwa. Kanuni ya
63 (3) inaelekeza kuwa ikiwa mbunge yeyote ataona kuwa Kanuni inakiukwa atasimama
mahali pake na kusema “kuhusu utaratibu”akiruhusiwa atataja kanuni iliovunjwa. Anaendelea kusema kuwa wakati anaongea hadi
kumaliza hakuna Mbunge au Waziri aliyefanya hivyo. Aidha, alieleza kuwa hakuna Kanuni
inayoelekeza kupeleka shauri kwa Spika ikiwa Mbuge ameshindwa kutumia Kanuni ya
63.
8.6 Mheshimiwa . Spika, baada ya maelezo hayo, Kamati
ilijiridhisha dhahiri kuwa Mhe. Anatropia Theonest (Mb) alikiri kuwa alisema
maneno yasiyo ya kweli ndani ya bunge.
Kwa maneno yake Mhe. Anatropia aliieleza kamati kuwa Mhe. William Lukuvi
(Mb) Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi hakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar
es salaam mwaka 2011, kwa hiyo, kwa vyovyote vile asingeweza kuhusika kupora maeneo ya
waathirika wa mabondeni wa Segerea na Ilala.
Mheshimiwa Spika, kamati inamtia
hatiani Mhe. Anatropia Theonest (Mb) kwa kusema uongo Bungeni kinyume na Kanuni
ya 63(1) na 64 ya Kanuni za kudumu za Bunge.
8.7 Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo na ufafanuzi huo sasa
tujielekeze katika hoja ya pili kuwa (b)
Ikiwa hoja (a) itathibitika, ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa na Bunge kwa
Mujibu wa Kanuni za Bunge.?
Katika Kanuni ya 63(8) inaeleza kuwa Mbunge aliyetakiwa kutoa
uthibitsho kwa kiwango cha kuliridhisha Bunge au atakataa kujirekebisha kwa
kufuta kauli au usemi wake Spika atamwadhibu kwa kumsimamisha Mbunge huyo ili asihudhurie
vikao vya Bunge visivyozidi vitano mfululizo kuanzia tarehe ambayo Taarifa hii
itawasilishwa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, Kamati ilizingatia masuala yafuatayo katika
kufikia mapendekezo ya adhabu:-
(i)
Mbunge huyo alitoa ushirikiano kwa Kamati kwa maana alipoitwa alifika
bila kukosa na alikiri kosa lake bila kupoteza muda wa Kamati.
(ii)
Kutokana na maneno aliyoyasema na kuufikia umma ni dhahiri
yalimdhalilisha Mhe. Lukuvi na kuharibu heshima yake katika jamii ya watanzania.
Kwa kuzingatia maelezo hayo Kamati inaliomba Bunge lako tukufu likubali
pendekezo la Kamati la kumsimamisha Mhe. Anatropia Theonest (Mb) na asihudhurie
vikao vitatu (3) vya Bunge mfululizo kuanzia tarehe 17 Juni, 2016 hadi tarehe
22 Juni, 2016.
Mheshimiwa Spika, Kamati inapendekeza adhabu hizi ili iwe
fundisho
kwake na kwa waheshimiwa wabunge wengine wasioheshimu na kutiii Sheria na
Kanuni za Kudumu za Bunge.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa, mapendekezo haya kuhusu adhabu
kwa Waheshimiwa Wabunge hawa itaenda sambamba na masharti ya Kanuni ya 75 ya
Kanuni za Kudumu za Bunge.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha, Kamati inapenda kueleza
kuwa adhabu zilizopendekezwa kwa Wabunge hawa zinaenda sambamba na Masharti ya
Kanuni ya 75 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, inayoeleza kuwa Mbunge
aliyesimamishwa kazi hataruhusiwa tena kuingia katika sehemu yoyote ya Ukumbi
wa Bunge na Maeneo ya Bunge kwa muda wote atakapokuwa amesimamishwa, na
atalipwa nusu mshahara na nusu posho zinazoambatana na mshahara huo.
8.0
HITIMISHO
9.1
Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kukushukuru wewe binafsi kwa
kunipa nafasi hii kuwasilisha maoni ya Kamati kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na napenda nitumie nafasi hii tena
kukupongeza kwa dhati kwa jinsi unavyoliongoza Bunge hili ambalo ni chombo cha
uwakilishi wa Wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ili kuhakikisha kuwa
ustawi wa wananchi unakuwa ndio kipaumbele cha kwanza.
9.2 Mheshimiwa
Spika, kipekee, nawashukuru Wajumbe wote wa Kamati, kwa kazi nzuri ya
kujadili na kuchambua kwa umakini mkubwa shauri hili kwani katika kutekeleza
jukumu hili walizingatia utaifa mbele na misingi ya haki. Kwa heshima naomba
niwatambue kwa majina kama ifuatavyo:-
(i)
Mhe. Kapt (Mst), George
H. Mkuchika, (Mb) - M/kiti
(ii)
Mhe. Almas Maige,
(Mb) -
Makamu Mwenyekiti
(iii) Mhe.
Rashid Ali Abdallah,(Mb)…………..Mjumbe
(iv) Mhe.
Amina Nassoro Makilagi, (Mb)…….Mjumbe
(v) Mhe.
Dkt. Christine G. Ishengoma,(Mb)……Mjumbe
(vi) Mhe.
Othman Omar Haji,(Mb)……………Mjumbe
(vii) Mhe.
Rose Kamili Sukum,(Mb)………………Mjumbe
(viii) Mhe.
George Malima Lubeleje,(Mb)………Mjumbe
(ix) Mhe.
Dkt. Suleiman Ally Yussuf,(Mb)……….Mjumbe
(x) Mhe.
Susan Anselm Lyimo,(Mb) ……………Mjumbe
(xi) Mhe.
Tunza Issa Malapo,(Mb)………………Mjumbe
(xii) Mhe.
Asha Abdallah Juma,( Mb)………….Mjumbe
(xiii) Mhe.
Augustino M. Masele,(Mb)……………Mjumbe
(xiv) Mhe.
Hafidh Ali Tahir, (Mb)…………………..Mjumbe
(xv) Mhe.
Innocent Sebba Bilakwate, (Mb)……Mjumbe
(xvi) Mhe.
Adamson E. Mwakasaka(Mb)……….Mjumbe
Aidha,
napenda kumshukuru kwa dhati Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas D. Kashililah, kwa
kuisaidia Kamati kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Kipekee, nawashukuru Ndugu
Pius T. Mboya, Kaimu Mshauri Mkuu wa Bunge wa Mambo ya Sheria, kwa ushauri wa
Kisheria walioutoa katika kuisaidia Kamati.
Aidha napenda kuwashukuru ndugu Matamus Fungo, Maria Mdulugu, Makatibu
wa Kamati, Lweli Lupondo, Sekretarieti upande wa Hansard na Editruda Kilapilo, msaidizi wa Kamati kwa kuratibu vyema
kazi za Kamati na kuhakikisha kuwa Taarifa hii inakamilika mapema.
Mheshimiwa Spika, mwisho
kabisa ni matarajio yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge wataipokea na kwa kauli moja
wataikubali hoja iliyopo mbele yetu ya matokeo ya taarifa ya Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge ya uchunguzi kuhusu Mhe. Suzan Lyimo na Mhe.
Anatropia kusema uongo Bungeni kwa nyakati tofauti kama tulivyoeleza katika
taarifa hii ili kuimarisha nidhamu ndani ya Bunge letu Tukufu na kuhakikisha
kuwa Kanuni za Majadiliano Bungeni, zinaheshimiwa na kuzingatiwa na Wabunge
wote.
Mheshimiwa Spika, naomba
kutoa hoja.
Kapt
(Mst) George H. Mkuchika, (Mb.)